Sababu za ugonjwa wa kifafa na Tiba yake

Sababu za ugonjwa wa kifafa na Tiba yake: Dalili, Sababu, Hatari, Utambuzi, Matibabu, Hatari, Ugonjwa wa kifafa ni ugonjwa sugu usioambukiza ambao huathiri ubongo na husababisha mtu kupata degedege mara kwa mara, yaani vipindi vifupi vya mishtuko wa mwili ambao unaweza kuathiri sehemu moja ya mwili au mwili mzima na wakati mwingine huambatana na kupoteza fahamu na kukosa udhibiti wa haja kubwa au ndogo.

Ugonjwa huu hujulikana kwa kitaalamu kama Epilepsy na unaweza kuathiri watu wa rika zote, bila kujali jinsia zao, rangi nk.

Kitaalamu ugonjwa wa Kifafa hutokana na hitilafu fulani inayotokea kwenye mfumo wa umeme wa ubongo ambapo shughuli za ubongo zinakuwa isivyo kawaida na kusababisha degedege au hali au hisia fulani zisizo za kawaida na wakati mwingine kupoteza ufahamu.

Aina Za Kifafa:

Kuna aina kuu mbili za ugonjwa wa kifafa ambazo ni pamoja na:

1) Primary Generalized Epilepsy.

Hii ndio aina ya ugonjwa wa kifafa ambayo inafahamika sana mitaani na inahusisha mgonjwa kukamaa, kupoteza fahamu, pamoja na dalili zingine kama vile kutoa povu mdomoni, na kujisaidia haja kubwa na/au ndogo bila kujitambua akishikwa na hali hiyo.

Pia wengine hupatwa kama na wazimu au kuchanganyikiwa kwa muda kabla au baada ya kushikwa na hali hiyo.

2) Partial Epilepsy.

Aina hii ya ugonjwa wa kifafa ni ile ambayo haihusishi muhusika kupoteza fahamu na kukakamaa bali hushikwa na hali fulani kama ya bumbuwazi kwa dakika kadhaa ambapo wengine huwa na dalili zisizoeleweka za mara kwa mara kama vile kuishiwa nguvu, kizunguzungu, kichwa kuuma sana (bila sababu ya kiafya inayojulikana) nk.

Aina hizi za kifafa ziko nyingi, na dalili hutofautiana kwa kadri ya aina ya kifafa.

Sababu za ugonjwa wa kifafa na Tiba yake

Sababu Za Ugonjwa Wa Kifafa:

Zifuatatzo ni baadhi ya sababu zinazomuweka mtu katika hatari ya kupata ugonjwa wa kifaa ambazo ni pamoja na:

1) Matatizo Wakati Wa Ujauzito Au Wakati Mama Anapojifungua.

Matatizo wakati wa ujauzito au wakati mama anapojifungua mfano ukosefu wa hewa (mtoto kuchelewa kulia), kiwango cha sukari kuwa chini kwa mtoto) yanaweza kuchangia kupata ugonjwa wa kifafa.

2) Maambukizi Ya Ubongo.

Maambukizi ya ubongo kama vile  uvimbe katika eneo la juu linalofunika ubongo (meningitis), kuvimba kwa ubongo (encephalitis), maambukizi katika ubongo yanayosababishwa na minyoo itokanayo na kula nyama ya nguruwe isiyoiva vizuri (neurocysticercosis) yanaongeza hatari ya kupata ugonjwa wa kifafa.

3) Sababu Za Vinasaba (Kurithi).

Aina fulani ya upungufu wa kijenetiki au hali ya kijenetiki yenye ulemavu wa ubongo unaohusishwa na ubongo kushindwa kufanya kazi inaweza kuchangia kupata ugonjwa wa kifafa.

4) Jeraha Kubwa La Kichwa.

Jeraha kubwa la kichwa litokanalo na aidha ajali hasa kwa waendeshaji wa vyombo vya moto barabarani kama vile bodaboda huongeza hatari ya kupata ugonjwa wa kifafa.

5) Uvimbe Kwenye Ubongo.

Uvimbe kwenye ubongo unaotengeneza saratani (brain tumour) unaongeza hatari ya kupata ugonjwa wa kifafa.

6) Kiharusi.

Ugonjwa wa kiharusi ambao hujulikana kwa kitaalamu kama stroke husababishwa na aidha damu kushindwa kupita vizuri kwenye mishipa inayouzunguka ubongo (ischemic stroke) au kupasuka kwa mishipa ya damu inayouzunguka ubongo (hemorrhagic stroke) hali ambayo husababisha mtu kupooza nusu ya mwili wake na huweza  kupata hatari ya kuugua ugonjwa wa  kifafa baadae.

Kumbuka:

Sababu za msingi za kifafa hazijulikani katika karibu theluthi mbili ya visa barani Afrika. Hii inaweza kuwa kwa sababu uchunguzi haufanyiki mara nyingi kutokana na upungufu wa rasilimali.

Dalili Za Ugonjwa Wa Kifafa:

Dalili za kifafa hutofautiana na hutegemea sehemu ya ubongo ambapo tatizo linaanzia, na jinsi linavyoenea. Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na:

1) Kutoa/ kukodoa/ kuchezesha kope za macho kwa sekunde chache

2) Kukakamaa au kutetemeka mwili mzima

3) Kupoteza fahamu kwa dakika/sekunde chache

4) Viungo kukamaa mfano kukakamaa kwa vidole vya mikono au miguu

5) Kuanguka ghafla na kuanza kutoa povu (frothy) mdomoni

Vipimo Vinavyofanyika Kugundua Ugonjwa Wa Kifafa:

Ugonjwa huu unaweza kutambulika kwa daktari kuchukua historia ya dalili zinazomkabili muhusika tu (hakuna kipimo ambacho kinaweza kutambua kifafa kwa asilimia 100) japo kuna kipimo kinachopima jinsi ubongo unavyotoa taarifa za umeme kiitwacho ELECTROENCEPHALOGRAM (EEG) ambacho kinaweza kutambua kifafa, lakini kipimo hiki kinaweza kikaonekana kuwa hakina shida, na bado mtu akawa na tatizo hilo la kifafa.

Hivyo basi, kifafa ni moja kati ya magonjwa machache ambayo kutambulika kwake kunategemea sana ujuzi na utaalamu wa daktari katika kuunganisha dalili za mgonjwa kuliko vipimo.

Hata hivyo, mara nyingi mgonjwa hupimwa vipimo tofauti ili kuweza kujua chanzo cha ugonjwa  mfano:

  • Kupima maji ya uti wa mgongo (lumbar puncture for cerebrospinal fluid analysis)
  • Kupima magonjwa ya zinaa hasa kaswende
  • Picha ya ubongo mfano CT SCAN

Matibabu Ya Ugonjwa Wa Kifafa:

Kifafa kinadhibitika kwa dawa au wakati mwingine kwa upasuaji.

Dawa (anticonvulsant drugs) zinaweza kusaidia kudhibiti degedege na kupunguza idadi za kutokewa na degedege.

Baadhi ya watu hutibiwa kwa kipindi chote cha maisha yao ili kudhibiti degedege, lakini kuna baadhi yao degedege huisha kabisa na kupona kifafa.

Vidonge Vya Kifafa.

Kifafa kinaweza kudhibitiwa ambapo hadi 70% ya watu wanaoishi na kifafa wanaweza kuishi bila kifafa kwa kutumia dawa za kuzuia kifafa ipasavyo zijulikanazo kwa kitaalamu kama antiepileptic drugs kama vile phenobarbital, phenytoin, gabapentin, pregabalin nk.

Kuacha kutumia dawa za kuzuia kifafa kunaweza kuzingatiwa baada ya miaka 2 bila kupata kifafa na inapaswa kuzingatia mambo muhimu ya kliniki, kijamii na kibinafsi.

Madhara Ya Kifafa:

Watu wenye kifafa hujikuta wamepata matatizo mengine ya kimwili kama vile mivunjiko na michubuko kutokana na majeraha yanayohusiana na kifafa, pamoja na viwango vya juu vya hali ya kisaikolojia, ikiwa ni pamoja na wasiwasi na mfadhaiko.

Vile vile, hatari ya kifo cha mapema kwa watu walio na kifafa ni hadi mara tatu zaidi ya idadi ya watu kwa ujumla, na viwango vya juu vya vifo vya mapema hupatikana katika nchi za kipato cha chini na cha kati na katika maeneo ya vijijini.

Kumbuka:

Mgonjwa wa kifafa  anapopata degedege na kushindwa kupata msaada mapema  ndivyo athari huongezeka na tatizo huwa kubwa zaidi. Hivyo inashauriwa mgonjwa mwenye degedege apatiwe huduma ya kwanza kisha apelekwe mapema hospitali au kituo cha afya kilichokaribu nae ili kupata msaada zaidi.

Jinsi Ya Kumsaidia Mtu Mwenye Kifafa:

Ukimuona mtu amepatwa na degedege, unaweza kuogopa, hasa ikiwa hujui nini cha kufanya. Kwa aina nyingi za degedege, hatua za msingi za huduma ya kwanza ndizo zinazohitajika. Hatua za kuchukua ni rahisi na mtu yeyote anaweza kuzifanya. Hatua za kumsaidia mtu mwenye kifafa ni pamoja na:

  • Mzuie mgonjwa asijiumize kwa kuweka kitu laini chini ya kichwa chake mfano mto, ondoa vitu vikali karibu yake kama kisu, sindano au vyuma ili visije vikamjeruhi
  • Weka kichwa cha mgonjwa alale anaangalia upande mmoja ili kutoa mate mdomoni
  • Usiweke kitu chochote mdomoni kwake kama vile maji, dawa, kibao au chakula mpaka mtu atakapopata fahamu.
  • Usimzuie anapokuwa akitetemeka
  • Kaa na mgonjwa mpaka degedege iishe na tazama degedege imedumu kwa muda gani
  • Mpeleke mgonjwa hospitali/kituo cha afya kilichokaribu nae kwa msaada zaidi
Jinsi Ya Kumsaidia Mtu Mwenye Kifafa

Mambo yanayoongeza hatari ya kupata degedege mara kwa mara kwa mgonjwa mwenye kifafa ni pamoja:

  • Kuangalia TV kwa muda mrefu
  • Kukosa usingizi kwa muda mrefu/kutopata usingizi wa kutosha
  • Mianga na miale ya disko
  • Unywaji wa pombe
  • Kuishiwa sukari mwilini kutokana na njaa kali
  • Kutomeza dawa za kifafa kama ilivyoelekezwa na daktari

See also:

  1. Sababu za Kukosa Hamu ya Tendo la Ndoa
  2. Sababu za Mwanamme Kukosa Hamu Ya Kufanya Tendo La Ndoa
  3. Sababu za Mwanamke Kukosa Hamu ya Kufanya Mapenzi
  4. Njia zinazotumika Kuondoa Harufu Mbaya Ukeni
  5. Zijue Dalili za Upungufu wa Nguvu za Kiume na Tiba Zake
  6. Vyakula vya kuimarisha misuli ya uume